Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Primary Question

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA K.n.y. MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kudhibiti mabadiliko ya tabianchi ambayo yamekuwa tishio kwa usalama wa viumbe?

Supplementary Question 1

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mheshimiwa Jacqueline ana maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; je, Serikali ina mpango gani wa kutoa ruzuku kwenye nishati mbadala ikiwemo majiko ya gesi pamoja na gesi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa maeneo yanayochimbwa madini kama makaa ya mawe pamoja na mchanga yanafukiwa au kurejeshwa katika hali yake ya asili kwa wakati na inavyostahili?

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alishiriki kwenye mjadala mmoja muhimu sana wa kitaifa ambao ulikuwa unazungumzia masuala ya kupunguza nishati ya matumizi ya kuni. Katika mjadala ule kuna maelekezo yalitoka tulipewa sisi Wizara tunaohusika na masuala ya mazingira na Wizara nyingine:-

(i) Tuendeleze kutoa elimu kwa wananachi;

(ii) Tunatakiwa tusimamie sheria, zipo Sheria za Mazingira; na

(iii) Tunatakiwa tuhamasishe wananchi wapande miti kwa wingi ili tuirejeshe miti ambayo ilishakatwa kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo alilolishauri la kuhakikisha kwamba tunaweka ruzuku kwenye matumizi haya ya nishati hasa gesi na nishati nyingine, tutalichukua tunakwenda kulifanya kazi kuona namna ambavyo tunakwenda kuhamasisha zaidi wananchi katika masuala ya kutumia nishati bora ya kupikia instead of kutumia kuni.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, tayari tulishatoa maelekeza kwa wachimbaji wote wa madini au wachimbaji wote wa makaa ya mawe kuhakikisha kwamba mashimo wanayoyabakisha baada ya kuchimba wayafukie. Pia tulishatoa maelekezo kwa Mameneja wetu wote wa NEMC wahakikishe kwamba wanawapa taaluma na taaluma wameshapewa wachimbaji wote wa makaa ya mawe ili kuweza kuepuka athari kubwa ya mazingira ambayo inaweza ikajitokeza hapo mbele.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Name

Mariamu Nassoro Kisangi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA K.n.y. MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kudhibiti mabadiliko ya tabianchi ambayo yamekuwa tishio kwa usalama wa viumbe?

Supplementary Question 2

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa mabadiliko ya tabianchi yanasababisha mvua kunyesha pasipo utaratibu na mafuriko pia. Je, Serikali imejipanga vipi katika kukabiliana na hali hiyo ya njaa pamoja na mfumuko wa bei katika nchi yetu? (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Mariam Kisangi hilo swali lako hapo mwishoni hebu litengeneze lirudi kwenye hoja yako kwa sababu mfumuko wa bei sasa utaelekea Wizara nyingine.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, mabadiliko ya tabianchi yanaathiri sana wakulima pamoja na makazi ya watu. Je, Serikali imejipanga vipi kukabiliana na hali hiyo? (Makofi)

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kumpongeza Naibu Waziri kwa majibu mazuri yote yaliyopita, lakini swali la Mama Mariam Kisangi ni swali la msingi sana.

Mheshimiwa Spika, Wataalam wa Idara ya Hali ya Hewa wanatuambia hivi sasa kiwango cha mvua maeneo mengine kimeshuka. Inaonesha wastani wa mita 1,500 sasa imefika mpaka mita 750, lakini tunakumbuka hivi karibuni tumekumbana na changamoto kubwa sana ya ukame katika Mikoa mbalimbali hasa Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Manyara. Katika hili ndiyo maana Serikali tumejielekeza kuelekeza suala zima la utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Ibara ya 238(L) kinachosema kwamba kila Halmashauri ipande miti milioni 1.5.

Mheshimiwa Spika, ninawashukuru Wabunge hawa na Watanzania na wadau wengine hatuna jinsi yoyote ya kupambana na hali hii, ni lazima tupande miti kwa kiwango kikubwa sana. Ninawaomba Watanzania wote tushirikiane na Serikali katika kulinda mazingira kupambana na mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. (Makofi)