Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Jacquline Andrew Kainja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kabla zahanati haijafunguliwa inawekewa vifaa tiba?
Supplementary Question 1
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza; kwa nini Serikali inapotenga pesa za majengo ya zahanati na vituo vya afya isitenge sambamba na pesa za vifaa? Kwa sababu mara nyingi majengo yanafunguliwa wakati vifaa hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; nini tamko la Serikali kwa majibu mazuri yaliyojibiwa hapa kwamba kuna pesa zimetengwa kwa ajili ya vifaa, tamko la Serikali katika Mkoa wetu wa Tabora kwa zahanati ambazo hazina vifaa na tayari wananchi wanachangishwa pesa za mabenchi kama Zahanati ya Goweko, Kalangale, Wilaya ya Uyui lakini vilevile Wilaya ya Igunga, Kagongo, Kata ya Itunduru na Ibuta - Kata ya Mbutu? Ahsante. (Makofi)
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrea, la kwanza, kwa nini Serikali isitenge fedha ya vifaa tiba kwanza; kimekuwa ni kipaumbele cha Serikali kujenga miundombinu kwanza ili huduma zile za msingi ziweze kuanza kutolewa na baada ya kuwa majengo yale yamekamilika na huduma za msingi kuanza kutolewa, ndipo Serikali inatenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na kuvipeleka kwenye zahanati hizo.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nilisema kwenye majibu yangu ya msingi, katika mwaka huu wa fedha ambao tunaumaliza, Serikali ilitenga shilingi bilioni 15 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba ambapo tayari bilioni 12.90 imeshanunua vifaa tiba hivyo na vimeanza kusambazwa katika zahanati zote nchini.
Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili; tamko la Serikali kwa zahanati kupata vifaa tiba katika Mkoa wa Tabora anaotoka Mheshimiwa Mbunge, Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele katika kuhakikisha vifaa tiba vinakuwa katika zahanati zote, vituo vyote vya afya vilevile katika hospitali za wilaya kote nchini katika kuhakikisha afya za Watanzania zinaboreka.
Mheshimiwa Spika, na kwa ajili ya kutekeleza hilo, Serikali imetenga shilingi bilioni 112 kwenye mwaka wa fedha 2023/2024 na vifaa tiba hivyo vitaanza kununulia mara moja mwaka wa fedha unapoanza, na tutaanza kuvisambaza katika maeneo yote nchini ya zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya, yakiwemo maeneo yale ambayo ameyataja Mheshimiwa Jaqueline Kainja.
Name
Shabani Omari Shekilindi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lushoto
Primary Question
MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kabla zahanati haijafunguliwa inawekewa vifaa tiba?
Supplementary Question 2
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru; je, ni lini Serikali itapeleka vifaa tiba katika zahanati za Wilaya ya Lushoto zilizokamilika?
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Serikali itapeleka vifaa tiba kwenye zahanati za Wilaya ya Lushoto pale ambapo tutaanza utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2023/2024 ambapo Serikali imetenga shilingi bilioni 112 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kote nchini.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved