Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Joseph George Kakunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Primary Question
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza: - Je, lini Serikali itafanya marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani ili kuweka tozo tofauti kulingana na ukubwa wa chombo cha moto?
Supplementary Question 1
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza niishukuru sana Serikali kwa usikivu na kusikia ushauri wetu sisi Wabunge, kama ilivyo kwenye Ibara ya 63(2), nashukuru sana.
Mheshimiwa Spika, sasa swali langu; je, Serikali itakuwa tayari wakati wanapokamilisha hiyo rasimu ya sheria kunikaribisha na mimi nitoe maoni yangu moja kwa moja?
Name
Sagini Jumanne Abdallah
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Butiama
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kama ilivyo ada ambapo utungaji wa sheria unahusisha wadau mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge na Kamati yako ya Kudumu ya Bunge, Mheshimiwa Mbunge kwa kweli ataalikwa na atashiriki katika hata hatua za mwanzo hadi sheria itakapokamilika, nashukuru. (Makofi)
Name
Kasalali Emmanuel Mageni
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sumve
Primary Question
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza: - Je, lini Serikali itafanya marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani ili kuweka tozo tofauti kulingana na ukubwa wa chombo cha moto?
Supplementary Question 2
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru; bodaboda maeneo ya vijijini ndiyo chombo kikuu cha usafiri kinachotumika kubeba wagonjwa kuwapeleka hospitali; na ili mgonjwa abebwe kwenye bodaboda inabidi abebwe mishikaki, awepo mtu wa kumshikilia, lakini Sheria ya Usalama Barabarani inazuia jambo hilo.
Nini tamko la Serikali juu ya watu wa vijijini wanaotumia bodaboda kupeleka wagonjwa hospitali? (Makofi)
Name
Sagini Jumanne Abdallah
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Butiama
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kiukweli ni hatari sana watu kutumia bodaboda kwa utaratibu wa mishikaki, na kwa mujibu wa sheria ni hatari kwa usalama wao na maisha yao, na nikiwa Naibu Waziri kwenye Wizara yenye dhamana ya usalama wa raia na mali zao, siwezi kutoa kauli ya kuhalalisha jambo ambalo linaweza likahatarisha usalama wa maisha wa wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, ushauri wetu, kama wanaona bodaboda ni chombo, kwa sababu ina magurudumu mawili, tunaweza tukashauri wakatumia chombo kilicho na magurudumu mawili kama baiskeli kuliko kutumia bodaboda ambayo katika kubadili gia, hawa wawili wote wanaweza wakajikuta wamedondoka na wakaathirika kiafya kinyume cha matarajio ya ndugu yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi nishauri tu kwamba tuendelee kuimarisha maeneo yetu na kwa namna ambavyo nchi yetu inazidi kuimarika, bila shaka muda mfupi ujao maeneo mengi yatakuwa na usafiri, kwa mfano magari ya michomko, yapo mpaka vijijini, japo hayaruhusiwi kubeba abiria, lakini tumeyavumilia kwa sababu ya mazingira yale, lakini kwenye boda boda ni hatari, hatuwezi kuruhusu jambo hilo.
SPIKA: Kwenye baiskeli ni sawa? (Makofi/Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nimesema baiskeli kwa sababu ya mwendo wa baiskeli, lakini kiti cha baiskeli kinabeba mtu mmoja tu. Mwendo wake ni mdogo, anatumia nguvu kazi ya yeye mwenyewe, lakini boda boda ni machine, ni engine sasa ile ni hatari kwa sababu ya ule mwendo wake na kadharika. Baiskeli kumbeba mgonjwa na ndio usafiri tumekuwa tukiutumia maeneo mengi ya vijijini. Tumetumia baiskeli za kwenda taratibu, lakini hii ya bodaboda ni hatari hata sio kwa mgonjwa hata wazima, tunawashauri wasitumie usafiri huo kama mshikaki.
SPIKA: Mimi nilitaka kuelewa tu sehemu ndogo, yaani kwamba kwenye baiskeli yule anayeendesha baiskeli akibeba watu wawili zaidi ni sawa?
NAIBU WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Hapana, kusudio langu abebe mtu mmoja na kile kiti kina uwezo wa kubeba mtu mmoja. Mwendo wake ndio nilisema kwa sababu ya tahadhari anayoisema Mheshimiwa Mbunge kwamba mgonjwa anatakiwa apate mtu wa kum-support kwa mwendo wa pikipiki hilo haliwezekani, lakini kwa baiskeli mwendo ule ni mdogo na familia nyingi zimekuwa zikibeba watu hao kwa baiskeli na wanafika, lakini sio pia mshikaki lakini hata kile kiti hakiwezi kubeba mshikaki.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved