Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:- Je, lini mkataba na mwekezaji utakamilika ili Mradi wa Liganga na Mchuchuma uweze kufanya kazi na kuchangia pato la Taifa?

Supplementary Question 1

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Swali la kwanza; lini Serikali italipa fidia ya Mradi wa Makaa ya Magangamatitu na Katewaka, Wilaya ya Ludewa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana ya kupitia upya Mradi huu wa Liganga na Mchuchuma, amekwenda mpaka China sambamba na kulipa fidia. Sisi tunataka kujua, majadiliano na mwekezaji yamefikia hatua gani, lakini tunataka kujua vile vile mkataba utasainiwa lini ili mradi huu uanze kufanya kazi? (Makofi)

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kuhusu suala la fidia kwa Mradi wa Magangamatitu na Katewaka kwa sababu tumeshaanza kulipa fidia kwenye mradi mkubwa, tukikamilisha zoezi hili maana yake zoezi litakalofuata ni kuangalia tena miradi hii ya Magangamatitu na Katewaka ili kuona nako fidia zinalipwa kwa wananchi wanaopisha miradi hiyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, Serikali inatambua umuhimu wa Mradi huu mkubwa wa Liganga na Mchuchuma ambao kwa kweli utakuwa na manufaa makubwa kwa Taifa letu. Kama alivyosema Mbunge, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anafanya kazi kubwa sana, Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia Diplomasia ya Kiuchumi tumeweza kufikia hatua nzuri sana kuweza kukamilisha majadiliano na hawa wawekezaji ambao mwanzoni walikuwa hawaji kwenye majadiliano.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimhakikishie kwamba juhudi zinazochukuliwa na Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha mradi huu unaanza mapema ziko kwenye hatua nzuri na tunaamini majadiliano haya sasa yatakamilika mapema kwa sababu nao wameanza kuonesha nia ya kutekeleza mradi bila kuleta vikwazo au vivutio vile ambavyo walikuwa wanadai mwanzo ambavyo vina hasara kwa Taifa letu, nakushukuru.

Name

Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Primary Question

MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:- Je, lini mkataba na mwekezaji utakamilika ili Mradi wa Liganga na Mchuchuma uweze kufanya kazi na kuchangia pato la Taifa?

Supplementary Question 2

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ikiwa haya ndiyo majibu ya Serikali.

Je, Serikali iko tayari sasa kutengeneza kitu kinachoitwa Program and Plan of Action kikionesha tarehe na miezi na mwaka kuelekea kuanzishwa kwa mradi huu badala ya kusema tu majadiliano yanaendelea? Watupe commitment ya Serikali. (Makofi)

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kama nilivyosema ni kweli tumekuwa na majadiliano ya muda mrefu na sababu kubwa ilikuwa ni upande wa pili kwa maana ya huyu mwekezaji ambaye kidogo alikuwa haji kwenye majadiliano kwenye vikao. Sasa kama nilivyosema, Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshaweka mahusiano mazuri na nje wanakotoka wenzetu wawekezaji hawa. Kwa hiyo tunaamini sasa kwa sababu wameshaanza kuja maana yake tutafikia muafaka karibuni, halafu tutatoa hiyo programu kwamba schedule ya utekelezaji wa mradi huu itakuwaje, nakushukuru.

Name

Christopher Olonyokie Ole-Sendeka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Simanjiro

Primary Question

MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:- Je, lini mkataba na mwekezaji utakamilika ili Mradi wa Liganga na Mchuchuma uweze kufanya kazi na kuchangia pato la Taifa?

Supplementary Question 3

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Naomba tu nimuulize Mheshimiwa Waziri. Kwa kuwa Mradi huu wa Liganga na Mchuchuma awali ulikuwa unaipa Serikali ya Tanzania 20% na 80% ilikuwa inakwenda kwa mwekezaji wakati uwekezaji wake ulikuwa ni dola milioni 600 tu kati ya dola bilioni tatu zilizokuwa zinahitajika. Je, Serikali imeweka mkakati gani wa dhati wa kuhakikisha kwamba sisi tunanufaika zaidi ukizingatia kwamba chuma cha Liganga ni jiwe ambalo liko juu wala huchimbi unafanya kukata tu kama keki ya harusi? (Kicheko)

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ni kweli mradi huu gharama yake jumla kwa tathmini za wakati ule ilikuwa ni bilioni tatu, mwekezaji huyu katika mkataba ule wa awali alikuwa awekeze kwa maana ya fedha kianzo dola milioni 600.

Mheshimiwa Spika, tunaamini katika majadiliano ambayo tunaendelea nayo sasa tutaona namna gani sasa kuhakikisha mwekezaji huyu anaweka fedha au mtaji wa kutosha ili sisi kama nchi tuweze kunufaika, zaidi katika mkataba huu hatuweki fedha yoyote lakini zaidi kupitia sheria zetu tutakuwa wanufaika wakubwa kwa sababu zile asilimia 20 ni interest ambayo sisi kama nchi hatuwekezi fedha bali kutokana na utekelezaji wa mradi huu sisi hizo ni asilimia ambazo tayari Serikali tunapata bila kuingiza mtaji wowote katika mradi huu.

Name

Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Primary Question

MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:- Je, lini mkataba na mwekezaji utakamilika ili Mradi wa Liganga na Mchuchuma uweze kufanya kazi na kuchangia pato la Taifa?

Supplementary Question 4

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, majibu ya Waziri yananipa wasiwasi, kwa sababu mimi nimekuwa Mjumbe wa Kamati ya Viwanda na inavyosemekana kwamba huyo mwekezaji wa kwanza ana matatizo na Serikali, inaonekana kwamba uwezo wake haupo. Sasa majibu ambayo anatupa Waziri ni ya Mkandarasi mwekezaji mpya au mwekezaji wa kwanza?

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ni kweli Mkandarasi huyu baada ya kutokutekeleza mradi huu kwa wakati kulingana na mkataba ule wa awali, Serikali tuliweza kufanya ufuatiliaji wa uwezo wa mkandarasi huyu. Kweli katika moja ya vitu ambavyo vilionekana ni kwamba alikuwa na uwezo mdogo, lakini baada ya majadiliano ya hivi karibuni amesema anaweza kufanya lakini bado tunaendelea kuona kama kuna mwekezaji mwingine ambaye anaweza kuwekeza baada ya kumalizana na huyu aliyeko mwanzo kama atashindwa.

Mheshimiwa Spika, katika majadiliano haya mojawapo ni kuona na kutathmini uwezo wa mwekezaji huyu wa mwanzo Sichuan Hongda na tukiona kwamba hana uwezo kulingana na taarifa ambazo tumezipata na vyanzo vya kutoka nchini kwake then tunaweza kutafuta sasa mwekezaji mwingine kulingana na utaratibu wa mkataba wa awali ambao lazima tuuvunje au tutafute namna nyingine ili kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa manufaa ya nchi. Kwa hiyo, haya yote katika majadiliano haya ya sasa hivi yanazingatiwa. Nakushukuru sana.