Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Maimuna Salum Mtanda
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Newala Vijijini
Primary Question
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: - Je, lini Serikali itaboresha miundombinu ya Chuo cha VETA Kitangari?
Supplementary Question 1
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, VETA Kitangari inahudumia majimbo mawili; Newala Mjini pamoja na Newala Vijijini, kwa hiyo, inasababisha usafiri wa wanafunzi kutoka kwenye maeneo yao kwenda katika eneo VETA ilipo ni mbali. Ujenzi ambao umetajwa na Serikali hauhusishi bweni la wavulana katika VETA hii.
Je, ni lini Serikali itaweka kwenye mpango ujenzi wa bweni la wavulana katika VETA ile ya Kitangari ili kuleta urahisi wa usafiri?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; linahusu watumishi, katika fani za umeme, ushonaji na uhazili, kuna mwalimu mmoja mmoja kiasi kwamba akipata dharura wanafunzi wale hawasomi.
Je, lini Serikali itapeleka walimu katika fani hizo, angalau mmoja mmoja, ili kuleta ufanisi na usomaji mzuri kwa wanafunzi katika VETA Kitangari? Ahsante.
Name
Omary Juma Kipanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Answer
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mtanda, Mbunge wa Newala kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwisha eleza kwenye majibu ya swali la msingi, kwamba katika mwaka huu wa fedha tumetenga shilingi milioni hizo 666 na katika fedha hizi tayari tumeshapeleka milioni 304 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa baadhi ya majengo. Kwa hiyo nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli ujenzi wa bweni ukawa bado kutokana na fedha iliyopelekwa. Lakini naomba nimhakikishie fungu lililobaki kati ya ile milioni 666 tutakapopeleka fungu hili la pili, ujenzi wa bweni hilo utakuwa umeanza na tutaendelea nao kwa kadri ya fedha tutakavyokuwa tunapeleka.
Mheshimiwa Spika, katika eneo la pili la watumishi, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu; Mheshimiwa Rais alitoa kibali cha kuajiri watumishi 514 katika mwaka huu wa fedha na mpaka sasa tumeshaajiri watumishi 169. Kwa hiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na eneo la Newala lakini tunafahamu tuna vyuo vya zamani na tuna vyuo vipya 25 vile vya Wilaya, vinne vya Mikoa tunakwenda kuwapangia walimu maeneo haya ili kuhakikisha kwamba taalum hii inaweza kutolewa katika maeneo hayo kwa uhakika, nakushukuru sana.
Name
Zuena Athumani Bushiri
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: - Je, lini Serikali itaboresha miundombinu ya Chuo cha VETA Kitangari?
Supplementary Question 2
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Chuo cha VETA Wilayani Rombo kwa kuwa Halmashauri imeshatoa eneo na wataalam wa ardhi wameshafanya uchambuzi na kuona linafaa?
Name
Omary Juma Kipanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Answer
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Zuena kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika ujenzi wa vyuo 68 vya wilaya zilizobaki, Rombo ni miongoni mwa Wilaya ambayo inakwenda kujengewa chuo hicho. Kwa hiyo, nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, kazi kule Rombo tayari imeshaanza. Tumefanya geo technical, topographical, environment impact assessment, na tayari tumeshatambua eneo na shughuli zimeshaanza katika mwaka huu wa fedha.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved